KITABU: UBATIZO WA KWELI KWA ULIMWENGU WOTE
Kitabu kimeandikwa na Mtume na Nabii Hebron Wilson Kisamo
UBATIZO WA KWELI KWA ULIMWENGUWOTE
YALIYOMO
1. UBATIZO NI NINI ?
2. UBATIZO WA KWELI
3. FAIDA ZA UBATIZO WA KWELI
4. HASARA ZA KUBATIZA KINYUME NA MPANGO
WA MUNGU.
5. JINSI MUNGU ANAVYOTAKA UBATIZO
UFUATWE
6. SALA YA TOBA
TOLEO LA KWANZA
9.8. 2012
ISBN 978-9987-9553-2-9
UTANGULIZI
Ndugu nakusalimu kwa jina la YESU KRISTO, ambaye ndiye Bwana na Mwokozi wa Mataifa yote, pia ndiye Mfalme wa wafalme na BWANA wa mabwana na hapana Mfalme mwingine zaidi yake. Mimi jina langu naitwa Hebron Wilson Kisamo, YESU amenichagua nimtumikie yeye kwa jinsi anavyotaka yeye ili kukomboa ulimwengu huu ambao umepotea na shetani ameumiliki kwa asilimia 98% sawa sawa na YESU alivyoniambia mwenyewe. Amenituma ulimwengu wote ikiwa inamaana nchi zote, mabara yote. Ujumbe huu aliniagiza rasmi na kunipa mamlaka yake tarehe 14.06.2010. Na akanipa jina la Kanisa lake niliite YESU NI BWANA NA MWOKOZI WA MATAIFA YOTE INTERNATIONAL MINISTRY. Akaniambia mwanangu nitautumia huu mwili wako kuukomboa ulimwengu wote, utachukiwa sana,utafanyiwa na kuitwa majina mabaya lakini usiogope tena ufurahi zaidi, kwani mimi YESU walinifanyia mabaya zaidi na ya uongo yakitokea kwa baba yao wa uongo ambae ni lusifa, nilifurahi daima.
Hakuna jambo lolote litakalofanikiwa juu yako au silaha yoyote juu yako, nipo na wewe milele. Nitakutumia kwa namna ya tofauti na kwa kiwango kikubwa sana ambacho hakijaonekana tokea kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu huu. Adui yako ni adui yangu, akasema YESU kwa sauti ya uchungu sana, watumishi wamenisaliti maagizo niliyowapa hawayafanyi na wamegeuza NENO langu kuwa maandiko badala ya Neno, maandiko yanatoka kwa shetani maana lusifa anaijua Biblia yote, na maandiko hayana uthibitisho wa nguvu zake YESU. Neno linatoka kwa YESU na lina udhihirisho wa nguvu za MUNGU. Napia wana wa adamu wanateseka wanalia na kuomba hawapati majibu, na zaidi wanazidi kupotoshwa na viongozi wa kanisa, maagizo niliyoyaacha nilivyokuwa ulimwenguni kabla ya kurudi kwa BABA yangu ili kuniandalia maandalizi ya ujio wangu ili nipate kuwaponya wengi waende mbinguni, imekuwa kinyume idadi kubwa ni ya watu wa shetani. Waliokuwa watumishi wangu wamenisaliti 98% sipo nao. Wameamua kwenda kuzimu, na shetani anawatumia na jinsi anavyowatumia, ni kubadili au kwenda kinyume na agizo la MUNGU, mfano watumishi kwa sasa wamefanya kanisa ni mahali pa biashara, kunyanganya watu vitu vyao na wakijua wamenitolea mimi, na kunifanya mimi YESU ndiye mnyanganyi, kwa midomo yao hunitaja kama wananipenda ila mioyoni mwao hawapo na mimi, wamekuwa watumishi wa pesa na sio mimi, wamekuwa wakitenda miujiza lakini siyo yangu ni miujiza ya shetani, na hao ni kati ya wale ambao siku ya mwisho nitawakataa na kuwaambia sikujui. Kanisa limeniacha kunitegemea mimi, imebaki 2 % tu ulimwengu mwote. Sasa mimi YESU ninalikomboa kanisa mwenyewe na ndipo unabii na utukufu wa kanisa la mwisho utakuwa mkubwa kuliko wa kanisa la kwanza unatimia sasa.
SHUKURANI
Namshukuru Mke wangu sana kwa kunitia moyo na kuniombea, nawashukuru watumishi wote wanaoniombea na kutumiwa na MUNGU kutumika pamoja na YESU aliyeniita, mkono wa MUNGU uwe juu yao siku zote za maisha yao. Asante.
MTUME NA NABII – HEBRON WILSON KISAMO
KIONGOZI NA MWANZILISHI WA HUDUMA
KANISA LA YESU NI BWANA NA MWOKOZI WA MATAIFA YOTE
INTERNATIONAL MINISTRY.
P. O. BOX 13657
ARUSHA, TANZANIA
EAST AFRICA
EMAIL: publications@prophethebron.org
1. UBATIZO NI NINI?
Ubatizo ni kiapo kati ya mwanadamu na MUNGU aliye hai, Aliye uumba ulimwengu pamoja na wewe ndugu msomaji wa kitabu hiki; Ubatizo ni agano lako wewe na MUNGU ya kwamba wewe ni wake wala sio wa mwanadamu au kitu chochote.
Ubatizo chanzo chake ni MUNGU mwenyewe ndiye aliyepanga akiwa anayo maana nzuri na njema sana kwa ajili ya mwanadamu ambaye ni yeye mwenyewe aliyemuumba kwa faida yake yeye mwenyewe MUNGU, moja wapo ya sababu amemuumba ili amuabudu yeye tu , na sio kitu kingine chochote, sababu nyingine akatawale kila kitu maana hivi viumbe vyote aliviumba ili mwanadamu avitawale ( Mwanzo 1:26 ). Baada ya anguko la mwanadamu shetani akauvuruga ulimwengu akijua kwamba ndiyo ameshinda na atatawala ulimwengu na wanadamu wote, baada ya haya kutokea. Ndipo MUNGU akaanzisha huduma ya ubatizo, ili kuwasafisha na kuwakomboa wana wa Adamu kupitia maji, kwanza kabisa MUNGU alimtuma Yohana aje ulimwenguni kuja kubatiza, Yohana ni mnaziri wa MUNGU aliyetoka mbinguni kama YESU alivyotoka mbinguni, akiwa Mbinguni alitumwa na Baba kuja kutengeneza njia yani YESU. Yohana 1 : 15 -18 ) . Na kabla ya ujio wa Yohana , nabii alitabiri juu ya Yohana na nabii Isaya alitabiri pia, na ikatokea. Yohana akazaliwa na Elizabeth na YESU ilitabiriwa hivyo hivyo na ikatokea, hawa wote ukiangalia hata jinsi wazazi wao walivyopata ujauzito ni kwa njia ya Roho Mtakatifu. ( Mathayo 1 : 18 – 24 ) , ( Luka 1: 11 – 38 ) Au kwa njia ya mpango wake MUNGU mwenyewe, ili kuukomboa ulimwengu huu, Yohana akazaliwa na akayatenda yale yote aliyoagizwa na MUNGU aje ayafanye ulimwenguni humu. Aliyafanya na alibatiza sawa sawa na alivyoelekezwa na MUNGU. (Mathayo 3 : 11 – 12 ) . Yohana alibatiza kwa maji ikiwa na maana kuwasafisha.
Ndugu msomaji wa kitabu hiki, natumaini mpaka sasa umeelewa ubatizo ni nini? Na chanzo chake ya kuwa ni MUNGU mwenyewe ndiye muanzilishi. Na wakati Yohana akibatiza mara nyingi alikuwa akielezea habari za YESU na pia kusema ya kuwa yeye ni mkuu sana hata yeye Yohana alikiri kabisa hastaili hata kuvichukua viatu vyake; Ndugu msomaji hapa hata Yohana alietoka mbinguni akatumwa ulimwenguni anakiri YESU ni Mfalme na yeye atabatiza kwa Roho na kwa moto ( Mathayo 3 :11 ). Na hata Yohana aliogopa kumbatiza YESU kwa ajili ya ukuu alionao lakini YESU akamwambia Yohana , Kubali hivi sasa ; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote, basi akakubali , na YESU alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini, na tazama mbingu zikamfunukia akamwona Roho wa MUNGU akishuka kama hua, akija juu yake, na tazama sauti kutoka mbinguni ikasema, “ Huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu ninayependezwa naye. ( Mathayo 3: 15 -17) . Ndugu msomaji na mtoto wa MUNGU tena umefanana na yeye MUNGU azidi kukufungua ufahamu wako zaidi ili uelewe zaidi kuhusu ubatizo aliouagiza MUNGU watu wote wabatizwe. Ukisoma katika injili ya ubatizo wa Yohana utaona ameyafanya yote aliyoagizwa na MUNGU ili tu wewe ukombolewe maana pasipo wewe kubatizwa huendi mbinguni ( Yohana 3 : 5-7 ) .
YESU alibatizwa kwa maji mengi na alibatizwa kwa maji mengi kwa maana ndivyo alivyoagizwa na akafanya kama kama yeye alivyotakiwa afanye na MUNGU, na YESU alikuja ulimwenguni ili kutukomboa na kwa sababu alikuja ulimwenguni kwa njia ya mwili ilimbidi na yeye abatizwe na kupitia ubatizo aliobatizwa na sisi sote tubatizwe kama yeye ambaye ndiye tunaemwamini na ndie njia ya uzima na ukweli. ( Yohana 14 : 6 ).
Na MUNGU alipo mtuma Yohana kubatiza, hakumwambia mtu akibatizwa awe na msimamizi mwanadamu, msimamizi wa ubatizo ni Roho Mtakatifu.
Utaona baada na hata kabla ya YESU kubatizwa hakuwa na mwanadamu msaidizi / msimamizi. Sasa mpaka hapa natumaini unazidi kuelewa kuwa katika ubatizo msimamizi ni Roho Mtakatifu na siyo mwanadamu,angalia mfano alivyobatiza Yohana na mpaka YESU alivyobatizwa na pia wale mitume wa YESU jinsi walivyobatiza, nao waliwabatiza watu bila wasimamizi wanadamu. Watu waliobatizwa walisimamiwa na Roho Mtakatifu tu, na ndio mpango wa MUNGU, mdhamini wa ubatizo ni Roho Mtakatifu. Lakini siku hizi agizo aliloagiza MUNGU limeachwa, siku hizi mdhamini wa ubatizo ni mwanadamu tena lazima awepo mwanamke na mwanaume. Huu sio mpango wa YESU ni mpango wa shetani ili kuangamiza watu wasiende mbinguni. Siri hii kaniambia YESU, waambie ulimwengu mzima hashiriki ubatizo huo ni feki. Baada ya ubatizo Roho Mtakatifu alimshukia YESU ili kumshuhudia ya kuwa ni mwana wa MUNGU na baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu, hapo ndipo YESU akaanza kuongozwa na huyo mdhamini ambaye awaushirika na MUNGU ( 100% ) akamwongoza kuyashuhudia matendo ya MUNGU, kumtia nguvu, mwana wa MUNGU. Hivi ndivyo inavyotakiwa katika ubatizo ni Roho Mtakatifu tu, siyo mtu asimamie mtu. Hayo ni mapokeo ya mwanadamu, ambapo baada ya YESU kupaa kwenda mbinguni shetani akawaingia wale ambao hawakumtii Roho Mtakatifu kubadili mpango wa MUNGU katika ubatizo. Na walibadili hata ubatizo wa maji mengi baadhi yao wakaanza kubatiza kwa kutumia beseni au kikombe tena ni vitone vya maji kichwani tu ! Nikuulize wewe je Yohana ndivyo alivyobatiza ? Jibu ni Hapana.
Na kama jibu ni hapana , hata kwa MUNGU ni hapana , na hata mbinguni ubatizo huo haupo na kama haupo mbinguni umetoka wapi ? Jibu ni kwa shetani, haijalishi jina la YESU linatajwa hata Roho Mtakatifu kutajwa , huo ni ubatizo feki. Ameniambia YESU niueleze ulimwengu wote ikiwa inamaana mataifa yote, watu wote wa rangi zote na kabila zote bila mipaka watu wajue ukweli wake na wamjue YESU wa ukweli, maana jina lake linatumiwa vibaya na watoto wake wanaangamia, kwa ajili ya watu walioubadilisha mpango wake MUNGU. Akasema mwanangu Hebron watoto wangu wananipenda sana ila hawambiwi ukweli kuhusu mimi 98% shetani ameuteka ulimwengu wote imebaki 2 % tu ndio wananijua kiukweli, sasa waeleze wabatizwe ubatizo niliobatizwa mimi YESU, watu wanajua kwamba mimi ndimi njia ya uzima na ukweli na hakuna atakayefika kwa Baba pasipo mimi YESU, na mimi YESU nilikuja ulimwenguni kuionyesha njia ya kwenda kwa Baba yangu, Baba yangu hakuwa mjinga kuagiza ubatizo wa maji mengi, hakuwa mjinga kumwambia Yohana mtu akibatizwa awepo na msimamizi. Leo hii nafasi ya Roho mtakatifu imechukuliwa na wanadamu, matokeo yake ni ubatizo batili, nakuuliza wewe unayempenda YESU je? YESU alivyobatizwa alikuwa na wadhamini? Jibu hapana. Hivyo ndivyo inavyotakiwa, mdhamini wako ni Roho mtakatifu na ndie atakae kuongoza na kukuombea maishani mwako na kukupeleka mbinguni.
Nakuuliza swali ili uzidi kufunguka ufahamu wako. Je ! mwanadamu ndie atakayekuongoza wewe ufike mbinguni ? Jibu ni hapana, ( Roho Mtakatifu ndiye atakaye kuongoza ufike mbinguni na kukushindia hapa ulimwenguni kama alivyo mshindia YESU ).
MUNGU hakuwa mjinga kutupa Roho Mtakatifu awe mdhamini katika ubatizo wake yeye, alijua kwamba, Roho Mtakatifu ana umoja na yeye au kwa lugha rahisi ili wewe uelewe, Roho Mtakatifu ni moja wapo ya nafsi ya MUNGU, Tunajua kwamba zote zina umoja ( MUNGU Baba, Mwana , na Roho mtakatifu ) na lile kusudi la kiapo cha ubatizo walipanga wote hawa watatu ili kukupata wewe, sasa nakuulizwa swali kama wewe haujadhaminiwa na Roho Mtakatifu utaenda wapi ? Jibu ni jehanamu. Badilika ubatizwe ubatizo kama YESU alivyobatizwa, Yeye ndio kweli na njia yake ifuatwe hakika utapona ( Yohana 4:6) usifuate mapokeo ya dini fuata mwongozo wa ubatizo ulioandikwa kwenye Biblia au kitabu kitakatifu cha MUNGU.
Safari yetu ya mbinguni na maelekezo yote yameandikwa ndani ya kitabu hiki na katika kitabu cha ufunuo wa Yohana 22 :18 – 19 MUNGU ameonya ole wake atakayeongeza au kupunguza ya nabii wa kitabu hiki, sehemu yake itaondolewa katika ule mji mtakatifu. Sasa ndugu msomaji embu chunguza kwenye Biblia kuanzia kitabu cha kwanza mpaka cha mwisho, hakika ( 100 %)
Hautakuta ubatizo wa maji ya kikombe yaani kichwa tuu ndio kiwekwe maji, hamna mdhamini mwanadamu katika ubatizo, sasa hapa utaona kabisa ubatizo umeongezewa mambo nje ya MUNGU alivyopanga na huu ni mpango wa shetani ili wewe usiende mbinguni. Maana tayari umeenda tofauti na y eye MUNGU. Ni kuulize swali je MUNGU ni mjinga aliposema mtu abatizwe kwenye kijito cha utakaso na azamishwe mwili wote? Jibu ni hapana.
Na je embu fikiria na ufunguke ufahamu wako uwe huru je! Kwa nini ni kichwa tu kinamwagiwa maji tena matone tu ! Je mpango wa MUNGU wa kuzama kwenye maji kama Yohana alivyobatiza umetimia ? na je huo mwili umeingia kwenye maji wote? Jibu ni kichwa tu kimemwagiwa maji na viungo vingine hamna kitu, sasa ujumbe huu amenieleza YESU na akanifundisha, kweli niliogopa sana baada ya kuujua ukweli halisi, akaniambia nilisha sema sana na baadhi ya watumishi wangu waseme kweli kwa mataifa yote, wamenisaliti, wananitaja tu jina langu midomoni mwao baadhi yao ni wanafiki, lakini ole wao mwisho wao umefika ni wakati wangu sasa mimi YESU nahitaji mwili wako tu kama nilivyoutumia mwili wa Paulo lazima watu wanirudie mimi na kazi hii ameianza YESU mwenyewe tokea (April 2012 ), Dunia nzima, na njia za kuzimu zote alinipa maelekezo ya namna ya kuzifunga kwa hiyo waliokuwa wanategemea kuchukua nguvu sasa hawana pa kuzipata wataporomoka mpaka (zero) haswa watumishi wanaotumia nguvu za giza. Hii ni kwa ulimwengu mzima na tayari wanajua mambo hayaendi.
2. BATIZO WA KWELI
Ubatizo wa kweli ni ubatizo aliouagiza MUNGU, uwe ni ubatizo aliobatiza Yohana na ubatizo aliobatizwa YESU tu. Huo ndio ubatizo ambao upo hata kwenye mafaili ya MUNGU na ndio anaoutaka. Na kama ubatizo uliopo mbinguni ni huu, basi ndio ufuatwe . Maana ndiyo anaoutaka na aliuandaa kwa ajili yako wewe ili upone, sasa kama umeukataa ubatizo alioutaka MUNGU na ukabatizwa ubatizo asio utaka yeye, haijalishi jina lake linatajwa huo ni ubatizo batili haumuhusu yeye, hayo ni mapokeo kutoka kwa waanzilishi walio mkufuru Roho mtakatifu , na wapo kuzimu.
Nilionyeshwa na YESU, tena dini zao ni kubwa kwa majina sana ulimwenguni.
Wamefungwa minyororo na YESU akaniambia hawa wanasubiri moto siku ya mwisho. Wamemkufuru Roho Mtakatifu, na wanateseka sana, walikataa kumtii MUNGU na wakamkufuru Roho mtakatifu, sasa wanakushangaa wewe unaengangania dini, unasema nitakufa na dini ya wazazi wangu ! Dini salama ni YESU tuu, ndio umtegemee yeye tu utapona.
Ubatizo wa kweli lazima taratibu zote alizofuata muasisi wa kanisa yaani YESU, ndizo zifuatwe ikiwa ina maana alichokifanya YESU ndiyo salama na ndiyo kweli na alifanya ili sisi tufuate njia aliyotuonyesha.
Mtoto mdogo abarikiwe tu kwa kuwekwa wakfu kama YESU alivyowekwa wakfu na kubarikiwa akiwa mototo, MUNGU aliandaa na kumpa ujumbe mtumishi wake Simon soma ( Luka 2 :29 ). YESU alipobarikiwa alikuwa mototo tena hajijui na alipokuwa mtu mzima au anao ufahamu ndio alibatizwa. Huu ndio mpango wa kweli na uliopo mbinguni na hata Yohana alitimiza na YESU akafanyiwa hivyo hivyo. Na kama unataka kuwa mfuasi wa YESU lazima ufuate taratibu zake hapo utakuwa kama yeye na utapokelewa na Baba yetu wa mbinguni, awafurahia na wazee 24 na malaika wake na serekali yake inafurahia.
Huo ubatizo mwingine hawafurahi kabisa, na ameniambia waambie wanangu wanielewe nawapenda.
3. FAIDA ZA UBATIZO WA KWELI
Unaanza kubarikiwa tokea ukiwa mototo mdogo kama YESU alivyobarikiwa akiwa mtoto. Na mtoto anakuwa mikononi mwa MUNGU, na MUNGU anaanza kumtengeneza kiroho na kimwili. Na mtoto atakuwa mwema na anatabia njema, na ndani yake anayo hofu ya MUNGU.
Unashiriki ubatizo alioutaka MUNGU Baba muumba wa vitu vyote ikiwamo na wewe, na unashiriki kiapo kamili kama YESU. Na zaidi utajazwa nguvu za Roho Mtakatifu kama YESU alivyoshukiwa na Roho mtakatifu ndiye anakuwa kiongozi wako milele na atakupeleka mahali alipo MUNGU kama YESU alivyopelekwa tena, kwa kushiriki hatua alizozitaka yeye mbingu inakuwa wazi. ( Yohana 3: 5- 7 ).
4. HASARA ZA KUBATIZWA KINYUME NA MPANGO WA MUNGU.
A. Hasara moja wapo wewe unakuwa umeshiriki jambo ambalo
halipo hata mbinguni na hata kwenye kitabu cha muongozo wa
kwenda mbinguni ( Biblia ) . Jambo lingine unakuwa umeshiriki
kuvunja amri ya MUNGU, ( Kumbukumbu la torati 5. 8 -9 ), 6: 14 -
16). Na pia unabeba laana maana unamjaribu MUNGU. Unatumia
jina lake na unafanya kinyume na yeye alivyotaka,na ukifanya
kinyume na yeye tayari unaabudu miungu mingine.
B. Mtoto anakuwa katika msingi usio wa MUNGU wa kweli, haijalishi jina la YESU limetumika. Mtu huyo ataishi kwa kushikiliwa na shetani na ndiyo maana unakuta mtoto hadi kufikia mtu mzima unajuta kwa nini umemzaa, anavuta bangi, anakuwa mwizi, mtukutu, ni mtu wa ajabu. Hii ni sababu ya kwenda kinyume . YESU alipelekwa kwenda kubarikiwa akiwa mtoto, sasa siku hizi mtoto anabatizwa kwanza, halafu akiwa mtu mzima ndio anabarikiwa ! Je, huu ndio mpango wa MUNGU?
Jibu ni hapana. Mtoto angewekwa wakfu kama YESU , haya mabaya yote yasingempata, angeanza na baraka, ndio msingi wake MUNGU. Hiyo ndio sababu moja wapo na shetani awashitaki kwa MUNGU. “ Si unaona hawafuati ’’ Japo yeye mwenyewe shetani anakutengenezea kosa ili uangamie na hapo hapo anakushitaki tena, ona jinsi shetani alivyomnafiki na ni mbaya sana.
C. Hasara nyingine huendi mbinguni unakuwa umeshiriki kiapo ambacho siyo kiapo amekitaka yeye MUNGU ili ukombolewe. Na MUNGU hakubali kiapo ambacho hakijatoka kwake! Nikuulize je wewe utakubali kusaini mkataba ambao haukuhusu? Jibu ni hapana, hutasaini. Hivyo ndivyo ilivyo kwa MUNGU.
D. Hasara nyingine ni ule wakati wa wewe kubatizwa ndio unapelekwa kubarikiwa ukiwa mtu mzima. Hasara unayoipata hapa majira yako ya baraka na ubatizo wa MUNGU kwako yanakuwa yamepitwa na wakati na MUNGU huenda na wakati, ndio maana kuna majira ya kupanda na majira ya kuvuna, kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka. Kwa hiyo haupati kitu kutoka kwake.
E. Wewe unakuwa ni wa dini na sheria tu.
F. Hautaki wokovu unakuwa mgumu maana nafsi yako imeshikiliwa na mapokeo ambayo hayajatoka kwa MUNGU na kama hayajatoka kwa MUNGU na kama hayajatoka kwa MUNGU ni ya mpinga kristo. Haiwezekani wewe ni mkristo halafu unapinga wokovu, ( Warumi 10: 9 -11) ina maana ndani yako ipo roho ya mapokeo ya dini na mapokeo ya mwanadamu, hawajui yametoka wapi, ni ya shetani na ile roho haimtaki YESU aingie ndani yako. Huu ni upofu ambao shetani ametumia njia mojawapo kuliteka kanisa na wewe unaekataa wokovu sasa, ufunguke uokoke. Kupitia ubatizo feki alioniambia YESU, mtu anakula kiapo na dini yaani yeye ni wa dini tu na siyo wangu na ndio maana mtu huyo hanitaki kabisa. Mtu huyo hatanikubali tu mpaka ile roho ya dini na mapokeo itoke ndani yake. Maana ndani yake ni roho ya kuasi inamshikilia. Na roho ya kuasi ikiwa ndani yake haijalishi ni kwa mtumishi au muumini, atashiriki pombe, tena hata atazibariki , atafanya uchawi, kuoa wake zaidi ya mmoja bila hofu ya MUNGU na hata ubarikio na batizo zao watashiriki vitu vya shetani.
Sasa nakuuliza , je ! YESU anashiriki hayo, au Roho mtakatifu anaruhusu disco kwenye sherehe za ubarikio au ubatizo? Jibu ni hapana. Kwenye hizo sherehe mapepo na roho mchafu ndio huja kushiriki na kufurahia ya kwamba mpango waliopanga wa kukuangamiza umetimia. Wacha sherehe za pombe, disco na mila.
5. JINSI MUNGU ANAVYOTAKA UBATIZO UFUATWE
a. Mtoto mdogo akizaliwa apelekwe madhabahuni awekwe wakfu tena iwe madhabahu ya kweli iliyo hai ambayo YESU anakaa hapo.
b. Mtu akiwa na ufahamu aokoke kwanza kwa hiari yake mwenyewe ndio abatizwe kwenye maji mengi tena yanayotembea. ( kijito cha utakaso) siyo kisimani.
c. Mwili wote uzamishwe kwenye maji kama YESU alivyobatizwa.
d. Angalia anaekubatiza awe kweli ana roho wa MUNGU ndani yake, maana kama ni roho wa shetani yupo ndani yake hawezi kukushirikisha ubatizo mtakatifu wa MUNGU, ( Hapo ubatizo ni feki ).
e. Ubatizwe kwa jina la Baba , Mwana na Roho Mtakatifu .
f. Usikubali kubatizwa kwa jina la mtu au kitu chochote tofauti na YESU
g. Usikubali kubatizwa na nabii wa uongo, hapo anakuwekea maraho yake na shetani aliye ndani yake ili akunajisi usiende mbinguni.
h. Usitoe pesa za malipo ndio ubatizo, YESU hakutoa na wewe fanya hivyo hivyo.
6. SALA YA TOBA
Kwa wewe ambaye hujaokoka na unapenda kuokoka.
UTASEMA MANENO HAYA:
Bwana YESU, nipo mbele zako naomba Rehema, unisamehe makosa yangu naomba uandike jina langu kwenye kitabu chako cha uzima wa milele; Bwana YESU nishike mkono, mimi ni wako kuanzia sasa . AMEN !
MUNGU akubariki sana akutunze, milele na Roho mtakatifu akuongoze mahali alipo YESU wa kweli ndio akupeleke hapo ukasali hapo. AMEN.
NOTE:
Ujumbe huu ameniambia YESU ni kwa watu wote wa ulimwengu huu. Na mtu yeyote ambaye amebatizwa kinyume na MUNGU alivyoagiza, waambie hawajabatizwa na mimi YESU sihusiki kabisa, maana ubatizo huo haujatoka kwa Baba yangu ni ubatizo wa mapokeo , haijalishi walitumia jina langu kama pazia hivyo hukumu inawasubiri. Injili yangu imebadilishwa,na ndio maana watoto wangu hawanioni, wamefungwa na shetani, na yeyote anae fanya kazi yangu kinyume na nilivyoagiza, tayari amekuwa nabii wa uongo, mtu yeyote akiongeza neno langu au kupunguza huyo ni mwongo, sina furaha naye hata Baba yangu na malaika wa mbinguni wote. Ole wao mwisho wao umeshafika. Narudi kuchukua ulimwengu na kuwakomboa wanangu mwenyewe. Na Tanzania ndio Edeni, mimi MUNGU nimeichagua , na Mataifa yote yataponea hapa na kunijua mimi YESU .
Haya ni maneno aliyo niambia YESU na nimeyanukuu kama alivyoniambia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni