BWANA YESU asifiwe, watu wote wa mataifa yote mlioubwa na Mwenyezi MUNGU na aliyetupa Neno lake lenye pumzi ili tulifuate na litufae katika wokovu wetu na ukristo wetu Mtakatifu. Ukisoma katika Kitabu cha 2 Timotheo 3:16-17, 16Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwabadilisha katika haki; 17ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
Utaona jinsi MUNGU alivyotupa andiko lenye pumzi yake ili utakapolifuata upate kuwa mtu kamili na kukuongoza wewe ili upate kufanikiwa na uwe na ushindi na uzima. Ninavyosema andiko lenye pumzi ya MUNGU nina maanisha ni Neno la MUNGU kama lilivyoandikwa bila kuchanganywa na uongo, yaani nuru na giza kutawala pamoja na kwa maana nyingine ni Neno la MUNGU kama lilivyo bila kubadilishwa na ndio sababu akaonya lisiongezwe wala kupunguzwa sababu alijua yale aliyoyaweka tayari yanatoka katika kinywa chake na hayo yatakayo ongezwa hayajatoka katika kinywa chake, hivyo hayana uzima kwa viumbe vyake na ikiwa hayajatoka katika kinywa chake hayana pumzi yake bali yana pumzi ya mungu asiyejulikana na anayaingiza ili kuuwa roho za wanadamu ili hao wanadamu wasifike mbele za MUNGU.
Nitaeleza mimi Nabii Hebron kwa ufupi baadhi ya mifano ya maandiko yenye pumzi ya MUNGU na kisha yakabadilishwa na mpinga kristo na mawakala wake ili kuwaongoza wanadamu na kuwatenganisha na Mwenyezi MUNGU kwa njia hiyo, hayo hufanywa na baadhi ya watumishi ambao wana ushirika na shetani na kuagizwa kuendeleza maandiko yenye pumzi ya shetani, mfano:
1. Ubatizo ni mmoja tu tena ni mtoni na ndio alioagizwa Yohana na YESU; Yohana akafuata ubatizo uliotoka katika kinywa cha MUNGU na ndio uliopo katika Biblia. Ubatizo mwingine wowote tofauti na huo haujatoka kwenye kinywa cha MUNGU. Ubatizo ambao hauna pumzi ya MUNGU ni wa kikombe, wa kisima, kubatizwa kwa jina la mtumishi. Sasa cha kujiuliza ni kwa nini ulimwengu umepotezwa na kufuata maandiko yasio na pumzi ya MUNGU na kumlazimisha MUNGU akubali yale ambayo hayajatoka katika kinywa chake ndio yafuatwe kama vile yeye MUNGU hajui kazi yake aliyoipanga au mwanadamu kutaka kumfundisha MUNGU wakati ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa? Hivyo basi yakupasa uelewe kuwa ubatizo wowote ambao ni tofauti na ule ambao alibatizwa YESU, yaani mtoni, ni batili (fake) na kama umebatizwa hivyo utakuwa umepokea ubatizo ambao MUNGU hajautaja na unapoupokea basi umebatizwa na miungu au mungu asiyejulikana na kukufanya kuwa mkristo asiye na MUNGU anayejulikana na hatimaye safari ya maisha ya mtu huishia kwa mungu asiyejulikana. Hivyo basi yakupasa kubatizwa kama YESU na kwa kufuata Kitabu chake na Sheria yake na siyo kwa kuleta sheria za kuwaongozea watu ambazo haziko katika Biblia Takatifu.
2. MUNGU anasema msiwatoze watu pesa mnapowaombea, soma Mathayo10: 7- 8. Lakini bado watu wanatozwa pesa za maombezi, unapo ona hayo uelewa kuwa ipo nguvu ya shetani ndani ya mtumishi huyo aidha ni wakala wa shetani anajificha kwa kutumia jina la YESU. Hebu muulize ni kwa nini unatoza pesa? Je! Ndivyo Neno lenye pumzi linavyosema? Hatakuwa na jibu!
3. Imeandikwa msiabudu sanamu, lakini utashangaa wakristo na baadhi ya watu wana abudu sanamu, sasa kuabudu sanamu sio neno aliloliamuru MUNGU, bali analikataa, ila watu wamekuwa na vichwa vigumu hawataki kumsikiliza MUNGU anavyotaka bali hupenda kufuata yale ambayo hayaja amriwa na MUNGU.
4. Imeandikwa nyumba ya MUNGU ni mahali pa sala tu, lakini utakuta inaitwa nyumba ya MUNGU ila ni mahali pa harambee, michango, matambiko, na baadhi ni sehemu za malango ya wachawi na shetani na kufanyia maagano ya makafara.
5. Kwa watumishi imeandikwa msijisumbukie, bali mniulize Mimi nami nitafanya, lakini wako baadhi ya watumishi huwalazimisha watoto wa MUNGU kutoa tena kwa lazima, na sadaka yako inakuwa ni deni na utafuatwa mpaka nyumbani au kazini. Hebu jiulize wewe unatoa sadaka au unalipa deni? Je! MUNGU wetu sisi ni MUNGU wa madeni au ni MUNGU mnyang’anyi? Jibu ni HAPANA. Yampasa mtumishi amuombe MUNGU na MUNGU atatenda, ila kwa wale watumishi waliojiita au kumwacha MUNGU au kujitengenezea utumishi kwa njia ya uganga, hao ni lazima wafanye hayo ya michango kupitia katika TV au radio au popote pale. Hebu muulize si imeandikwa msijisumbukie maana nyie ni bora kuliko maua na mbona wanafanya hivyo na hilo sio neno lenye pumzi ya MUNGU? Hawatakua na jibu!
Ukiwa msomaji mzuri wa Biblia, utajua mambo mengi yanayofanywa na baadhi ya makanisa au baadhi ya watumishi katika dunia hii kwa kiwango kikubwa utafahamu ya kuwa MUNGU anachukiwa na wala haheshimiwi bali shetani anatukuzwa sana kwa maandiko yake yasio na pumzi ambayo yanatumika katika baadhi ya makanisa, lakini nataka uelewe kuwa sio kila kanisa au kila mtumishi anayetumia jina la YESU ni wa kweli au ni makanisa ya kweli. Makanisa au watumishi wa kweli wamebaki wachache sana, wengi wao aidha mmoja mmoja au kwa umoja wao wako kipesa au kibiashara na wengine wametumwa na shetani kuangamiza roho za wanadamu ili unapowafuata au unapofuata elimu yao, yenye michanganyo na uongo basi unakuwa umepotea, jinsi alivyo kuhani ndivyo walivyo na kondoo wake.
Zaidi fuatilia YouTube za Prophet Hebron kupitia www.prophethebron.org, utajifunza mengi na kuokolewa, ni wakati sasa wa kila mtu ambaye anampenda MUNGU akatae kabisa kupokea maandiko yasiyo na pumzi ya MUNGU, unapoyapokea tu unakuwa umekufa kiroho, ila sasa ipo neema, pokea na kufuata Neno lenye pumzi ya MUNGU, uchukue hatua ili ufufuke, sababu ulikuwa umekufa kiroho na katika ulimwengu wa roho, MUNGU hakujui japo wewe utaona kuwa unampenda ila ulikuwa umepotezwa ukaletewa mapokeo ya wanadamu, soma Mathayo 15:6-9.
Sema: Bwana YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote ikiwemo na dhambi ya kupokea mafundisho yasiyo na pumzi yako, namkataa shetani na mafundisho yake na kazi zake, naomba uandike jina langu katika Kitabu chako cha Uzima wa Milele na naomba Neema ya kupokea mafundisho yenye pumzi Yako. AMEN.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni