Wafilipi 2:10-11
  • ZIJARIBU HIZO ROHO! JE NI ROHO ZA MUNGU WA KWELI AU ZA mungu WA UONGO?


    BWANA YESU ASIFIWE, YESU wa Nazareti aliye hai.

    1 Yohana 4: 1-3

    “ Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. 2 Katika hili mwamjua Roho wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. 3 Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.”


    1.  Katika somo hili kama alivyonifundisha YESU mwenyewe mimi Hebron kabla ya kuanza kazi yake ya kumtumikia. Hapo mwanzo sikuyajua haya na mengi zaidi lakini alinifundisha ili niwaeleze na kuwafundisha watu wote wa ulimwengu ili wamrejee yeye YESU, kwa sababu wapo wengi wasiyoyajua haya kwa kuwa tayari wameshatekwa na shetani, ingawaje hawampendi shetani lakini wamepigwa upofu. Nitaelezea kwa ufupi ila zaidi nimeelezea somo hilo katika YouTube (www.prophethebron.org).

    Hapo mwanzo mimi nilifikiria ukishajiita mkristo na ukaokoka tayari wewe ni mkristo wa kweli kumbe siyo hivyo. Ukisoma mstari wa pili kuwa kila mtu anayemkiri YESU kuwa imetokana na MUNGU, hiyo haitoshi sababu hata mashetani yanaamini hivyo. Kinachotakiwa hapo ni kuokoka na kuachana na dhambi. Hapo awali niliamini YESU ni mwana wa MUNGU lakini sikuwa nimeokoka, hivyo sikuwa na tofauti na yule asiyemjua YESU kabisa wala mwenye ushirika na yeye bali nilikuwa na ushirika na yesu wa uongo au mpinga kristo kwa sababu yeye ndiye anayewawekea watu roho ya kukataa kuokoka ili wawe chini yake na apate wafuasi wa kuchomwa pamoja naye katika ile mwisho.

    Nilikaa katika ukristo wa kuwa muumini wa mpinga kristo pasipokujua wala kupenda kwa sababu nilizaliwa nikayarithi kutoka kwa wazazi wangu ambao na wao pia walirithi pasipokujua wala kupenda. Ikafika wakati nikaokoka nikapata utamu wa YESU na nilimpenda sana na yeye anajua na katika kuokoka kwangu nilisali katika makanisa, yapo baadhi yaliyokuwa na YESU wa kweli na mengine hayakuwa na YESU wa kweli na mengine YESU wa kweli alikuwepo lakini baadae akaondoka. Pale nilipomkuta YESU ndipo aliponichukua na kunimiliki ila akaondoka mahali pale kwa sababu YESU alifukuzwa kwa matendo potofu (kwa sababu kweli iliondolewa, mtumishi akaanza uongo na wivu pamoja na mabaya yasiyofaa. Hata kujiita yeye ni MUNGU ili kanisa limwabudu yeye na hata ikawa hivyo na hapo mimi nilikataa kabisa). YESU wa kweli akaniongoza nisiende kanisa lolote bali nikae nyumbani kwa miaka miwili akinifundisha yeye mwenyewe. Nakuja katika hoja ya msingi (point) hapa; zijaribuni hizo roho kama zinatokana na MUNGU.

    Jinsi ya kuzijaribu nitaelezea kwa ufupi, kwa ufahamu zaidi fuatilia masomo yangu utaelewa zaidi. Maana ya kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU maana yake ni hii; Mtu anaweza tumia jina la YESU kuhubiri lakini ndani yake siyo roho ya MUNGU itendayo kazi bali ni roho ya shetani. Mfano; ubatizo wa kikombe, ubatizo wa kisima, ubatizo wa maji mengi kwa jina la mchungaji. Mahali hapo hata kama watu wanaponywa na wameokoka, hizo batizo si za MUNGU kabisa wala hizo kazi siyo za kuzaa matunda ya MUNGU ni za kuzaa matunda ya shetani.

    Imeandikwa katika Ufunuo 22: 18-19 mtu asiongeze lolote katika kitabu kitakatifu wala kupunguza; sasa zichunguze hizo roho, je ni roho za MUNGU? Jibu unalo, na hii ni kwa dunia yote. Tafuta katika biblia kitabu cha mwanzo hadi cha mwisho hakuna mahali batizo za aina hiyo zimeandikwa, basi unapozipokea unawekwa wakfu na roho ambazo hazitokani na MUNGU wa mbinguni bali na mungu asiyejulikana, hivyo madhara yake kila unapo omba au utoapo sadaka zako au toba zako wewe unakuwa umemwabudu huyo mungu asiyejulikana bila kujua au kupenda japo wapo baadhi ya viongozi wanajua kabisa wanafanya kazi ya shetani ya kuwapoteza watu wasiende mbinguni.

    2.  MAOMBI YA KUTOZWA PESA

    Imeandikwa “nimekupa bure, toa bure”, sasa ikiwa unadaiwa pesa kwa ajili ya kuombewa au utoe pesa fulani ili ukae katika kiti uombewe labda na nabii au yeyote yule. Napenda kuwaeleza ulimwengu wote, haijalishi jina la YESU linatajwa na huyo mtu, ukweli ni kwamba yeye haongozwi na roho wa MUNGU wa mbinguni bali ni roho wa shetani anajificha kupitia yeye ili kunyang’anya watu mali zao. Hao ni waongo na lengo lao ni kuupoteza ulimwengu huu. Angalia neno la MUNGU linavyosema na yeye hawezi kuwa kigeugeu alibadilishe neno lake.


    3.  MADHABAHU INAYOONGOZWA NA ROHO ZA SHETANI LAKINI WANALITAJA JINA LA YESU MAHALI HAPO.


    a.         Mambo ya dunia hii yakichanganywa na ya mbinguni hupatikana mahali hapo ili kuwapiga watu upofu wajione wapo na MUNGU wa kweli. Mfano pombe ni halali mahali hapo, sanamu ni halali, ibada za wafu ni halali kabisa. Ukisoma neno la MUNGU linayakataa mambo hayo sasa wewe hauoni huko ndiko kumkataa MUNGU na kumpeda shetani? Zijaribu, jibu limepatikana sasa.

    b.        Madhabahu kuchimbiwa vitu vya waumini, makafara, kuzindikwa kwa uchawi, hata kama mtaabudu yesu wa uongo mambo hayo ni ya giza, hakuna ushirikiano kati ya giza na nuru.

    c.         Kusoma majina ya watu wanaotoa fungu la kumi na kuwapa vyeti au kupewa risiti za kumbukumbu (memory) za kutoa au kuchangisha pesa katika ibada, hayo yote ni machukizo mbele za MUNGU bali hayo yote ni shangwe kwa shetani. Tazama kipindi chake YESU, aliyakuta mambo ya dunia hii yaliletwa kanisani na yale ya mbinguni yakaondolewa na hata sasa ndivyo ilivyo na ndiyo ukweli kabisa, mambo ya mbinguni yanayotakiwa kufanyika katika nyumba ya sala yanaondolewa na badala yake mambo hayo ya aibu ya dunia hii ndiyo yapo sehemu nyingi katika dunia hii na huku ndiko kuipenda dunia. Kanisa likipenda dunia haliwezi kumsikia MUNGU, hivyo ya nini kujichosha, sasa muelewe. Zijaribuni hizo roho yaani hayo yanayofanyika na mengineyo mengi, je ni ya neno la MUNGU? Siyo.


    d.        KIKAPU CHA MAMA MCHUNGAJI.

    Hii ni roho ya pepo la kike ya unyang’anyi ikiingia kwa mke wa mchungaji ni lazima afanye hivyo na inaingia kwa kanisa kulinajisi. Jaribu hiyo roho; wewe unamtolea MUNGU sadaka au mama mchungaji?



    e.         ROHO YA WATUMISHI KUTAFUTA PESA.

    Imeandikwa “mtumishi wangu usisumbukie utakula nini, katika kila jambo nieleze mimi nitafanya.” Hii roho ya michango ina maana ni umasikini. MUNGU kazi yake inafanywa na sadaka zinazotolewa yeye ndiye anazozijua au pale mtu anapoamua kufanya jambo fulani kwa ajili ya MUNGU pasipo kuchangishwa tena ajisikie yeye mwenyewe ndani ya moyo wake na BABA yake ataujaza moyo wake.


    Katika vipindi vya radio, tv, magazeti, n.k. utasikia na kuona matangazo ya kuchangisha, utasikia tutumie kwa namba hizi, hiyo ni roho isiyotokana na MUNGU; kama vipindi ni vyake MUNGU mwenyewe atafungua njia pasipo mtumishi kuanza kuomba pesa kwa watu au kujiaibisha kuwa yeye anaongozwa na mungu asiyeweza au masikini, wala usishangae ukweli ndio huo, huko ndiko kuzijaribu. Je hizo roho zatokana na mungu? Jibu unalo.

    Yapo mengi, nakuombea wewe unayesoma Roho Mtakatifu akufunulie mengi ili ujijue zaidi usije ukaongozwa na roho za shetani za dunia hii na kukufanya wewe ni wa dunia hii. Mfano mwingine utaona MUNGU yeye mwenyewe katika neno lake anasema usitoze riba lakini sasa utakuta kanisa lina benki na wewe unajua benki inatoza riba ili iendelee lakini hapo hapo utaona miujiza ikitendeka na jina la YESU likitajwa. Sasa jiulize je hiyo roho ya benki katika kanisa ni roho ya YESU? Zipo nyingi zinajificha zikiwemo uzinzi, ulevi, makafara, waumini kufa vifo vya ajabu na mengineyo ya ajabu. Unaweza ukaona unafanya kazi ya YESU kumbe unafanya kazi ya shetani japo wapo wanaojua kabisa wanafanya nini na wanamtumikia nani.


    Sema; BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu uandike jina langu katika kitabu chako cha uzima wa milele na hizo roho za dunia hii zitoke ndani yangu katika Jina la YESU wa Nazareti wa mbinguni.

                                                                                                 

    NABII HEBRON.

    Hakuna maoni:

    Visits

    Translate