Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde: Napenda nikushirikishe ushuhuda wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni katika wakati huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho pale tunapoomba. Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa. Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na
wachawi wa kawaida. Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA. Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje huko na kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling) . Na kijana huyu alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi. Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye kanisa
hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile. Siku moja, kijana huyu aliuacha tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho. Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake. Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na
mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika. Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua." Mchungaji alipofungua macho yake, alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye; maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi aliingia, isipokuwa tu malaika
walimpitishia kwenye paa. Sasa, mambo haya ni magumu kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?" Kijana yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka. Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili. Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine. Usiku mmoja, mimi (John Mulinde) nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema,
alitoa ombi. Kulikuwako na wachungaji wengi pale kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni watu namna ya kuomba." Watu ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni watu namna ya kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa." Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na mapepo haya yanaweza
kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza kuathiri matukio yanayoendelea duniani. Pale mapepo wachafu pamoja na maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara. Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi
yote huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni. Baadhi ya maombi huonekana kama moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani. nyingine ya maombi nayo ni kama moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa, lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea. Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu anapoomba. Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo na kuendelea hadi juu. Mara nyingi
watu wanapoanza kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba yanapenya kabisa ule mwamba. Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!" Mara nyingi Wakristo hushindwa na mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi. Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja niende
nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi. Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu, bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao. Na kama watu waking'ang'ana kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza kustahimili
pia. Wote wanakimbia. Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha kuburudisha, na chenye nguvu. Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi. Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu linabakia wazi. Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu
linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba, katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao. Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo vyote vya adui vinadhoofika. Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo. Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili
ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa na nguvu sana. Na kama kuna sehemu ambako maombi ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika. Na kama atatokea mtu wa kusema nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena kwenye sehemu kama hizo. Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo? Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi. Sasa unaweza kupiga picha, sote tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu
akieleza ushuhuda wake. Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri. Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa." Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana. Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la
hasira, basi adui atasababisha watu watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi, anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana, lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii tena! Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika! Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu
wako. Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, "Hii si vizuri kabisa." Kumbuka tu Biblia inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu." Kila mara unapopata mpenyo katika maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana, nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia, usiniongoze kwenye majaribu.
Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali fulanifulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee, Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu." Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako kwa Kristo, wewe sema tu, "Asante Yesu." Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika, "Mshukuruni Mungu kwa kila jambo." Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa njia hiyo anatuokoa na mambo yapi, tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo. Yule kijana aliendelea kusema kuwa, unapopata mpenyo katika maombi,
majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya maombi yake. Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14) . Alisema kuwa watu wanapoomba, majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana. Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha
za kiroho na amejivika silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika kikamilifu kwa silaha hizohizo. Lakini, kama anayeomba hajali silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana. Malaika anapokuwa anakuja, mapepo wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni. Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini; mimi narudia tu kile ambacho
kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza, "Je, malaika wanaweza kuungua moto?" Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi. Kumbuka kile ambacho Biblia inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho. Katika Biblia, Yesu alisema, "Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea?
Au utakata tamaa na kumwacha adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea? Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye. Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo, Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho. huyo, "Una maana kuwa malaikaNilimwuliza kijana anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?" Sasa alikuwa anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na malaika wa nuru kwa mtu huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi
mabaya. Na mara nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina. Niliondoka kwenye kile chakula cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, "Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini jambo hili." Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi. Alinipa mambo matatu: Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba yetu. Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile
kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu sisi. Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia, anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, "Omba." Wewe unasema, "Hapana! Muda wangu haujafika." Na anasema, "Omba sasa!" Kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Wakati mwingine anasema, "Kesho ni kufunga." Wewe unasema, "Hapana, nitaanza Jumatatu!" Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye
njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili, linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali ni vya Bwana! Haleluya! Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu, kisha tu muambiane, "Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote." Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi! Asante Yesu. ********************** *°·.¸¸
UNABII WA KWELI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni